Friday, July 31, 2015

Simba Imeshinda katika mchezo wake wa Pili wa Mazoezi dhidi ya Timu ya Black Sailor kwa mabao 4--0

Kikosi cha Timu ya Black Sailor iliopanda daraja mwaka huu kucheza Ligi Kuu ya Zanzibar kwa Msimu wa mwakac 2015/2016, ilikubali kupigo cha mabao 4--0 dhidi ya timu ya Simba katika mchezo wa kirafiki uliofanyika usiku huu katika uwanja wa amaan Zanzibar. 
Kikosi cha Simba kilichotoa kipigo kwa Timu ya Black Sailor uwanja wa Amani usiku huu Simba ikiwa Zanzibar kwa michezo ya kirafiki kuimarisha Kikosi chake kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania. 
       Jopo la Makocha wa timu ya Simba wakifuatilia mchezo huo wa kirafiki na timu ya Black Sailor
Mchezaji wa timu ya Simba akikokota mpira akijiandaa kumpita beki wa timu ya Black Sailor, wakati wa mchezo wao wa kirafiki uliofanyika uwanja wa amaan timu ya Simba imeshinda 4--0
Mchezaji wa timu ya Black Sailor akiwapita wachezaji wa timu ya Simba katika mchezo wa kirafiki.
                    Mshambuliaji wa timu ya Simba akimpita beki wa timu ya Black Sailor

Mchezaji wa timu ya Simba Abdi Banda akiifungia timu yake bao la kwanza kwa kichwa katika mchezo huo wa kirafiki uliofanyika uwanja wa Amaan timu ya Simba imeshinda bao 4--0
Wachezaji wa Simba wakishangilia bao lao la kwanza lililofungwa na mchezaji Abdi Banda kwa kichwa baada ya kupigwa krosi na Khamis Kiiza, mwenye jezi namba 5
Mshambuliaji wa timu ya Simba akimpita beki wa timu ya Black Sailor wakati wa mchezo wao wa kirafiki.
              Mshambuliaji wa timu ya Simba Khamis Kiiza akimpita beki wa timu ya Black Sailor


Mshambuliaji wa timu ya Simba na Black Sailor wakiwania mpira wakati wa mchezo wao wa kirafiki uliofanyika uwanja wa Amaan Zanzibar timu ya Simba imeshinda 4--0 mchezo uliofanyika usiku huu.
Mshambuliaji wa timu ya Simba akizuiya mpira huku mabeki wa timu ya Black Sailor wakijiandaa kumzuiya.
       Kipa wa timu ya Black Sailor akidaga mpira ikiwa moja ya ulio gplini kwa timu ya Black Sailor
Mshambuliaji wa timu ya Simba akiruka kiunzi cha beki wa timu ya Black Sailor wakati wa mchezo wao wa kirafiki uliofanyika uwanja wa Amaan Timu ya Simba imeshinda 4--0
Goli la pili la timu ya Simba lililofungwa na mshambuliaji Ibrahim Hashim katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo wa kirafiki uliofanyika uwanja wa amaan timu ya Simba imeshunda 4--0
                           Beki wa Timu ya Black Sailor akiokoa mpira galini kwake
Mchezaji wa Simba akiwa juu akipiga kichwa golini kwa timu ya Black Sailor.
Beki wa timu ya Black Sailor akioko mpira golini kwake wakati wa mchezo wa kirafiki uliofanyika katika uwanja wa Amaan Timu ya Simba imeshinda 4--0.
Picha na OthmanMapara.Blog. Zanzinews.com  

FOMU ZA WAGOMBEA URAIS ,UBUNGE PAMOJA NA UDIWANI KESHO-LUBUVA

 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),Jaji Mstaafu,Damian Lubuva (katikati) akizungumza na waandishi habari juu juu ya maendeleo mbalimbali katika kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika leo Makao Makuu ya NEC jijini Dar es Salaam,Kulia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishina Suleiman Kova na Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Uendeshaji Uchaguzi,Clothilde Komba.
 Kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,Kamishina Suleiman Kova akizungumza na waandishi habari juu juu  jeshi la polisi lilivyojipanga katika suala la ulinzi kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika leo Makao Makuu ya NEC jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa habari wakifatilia wa taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,Jaji Mstaafu Damian Lubuva leo Makao Makuu ya NEC jijini Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Massaka wa Globu ya Jamii) 

Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kuanza kutoa fomu ya urais ,Ubunge pamoja na Udiwani kesho na kumalizika kwa zoezi la utoaji fomu hizo ni Agasti 21 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,Jaji Mstaafu,Damian Lubuva  amesema wakati wa uchukuaji wa fomu ya urais itatolewa bure lakini wakati wa kurudisha anatakiwa kuweka dhamana ya Sh.milioni Moja na wadhamini wadhamini 200 katika kila mkoa na kuwepo kwa mikoa miwili Zanzibar.

Lubuva a amesema kuwa wakati wa kuchukua fomu viongozi wa vyama vya kisiasa wanatakiwa kuchukua fomu na kurudisha bila kuwa na kundi kubwa ambalo linaweza kusimamisha shughuli za watu wengine.

Amesema kwa fomu za ubunge ni sh.50,000  na udiwani sh.5000 ambapo wanatakiwa kuchukulia katika ofisi za wilaya na uchukuaji huo lazima uwe wa kistaarabu katika kuweza watu wengine waendelee na shughuli zao.

Lubuva amesema kuwa  wanasiasa wanatakiwa  na lugha za kistaarabu katika mikutano yao katika kujenga demokrasia iliyo ya ukweli.

Hata hivyo amesema kuna baadhi ya vijana wanauza kadi za tume ya taifa ya uchaguzi na kutaka vyombo vya usalama kuchunguza pamoja na kuwachukulia hatua watu wanaouza kadi hizo.

Kamanda wa Polis wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishina Suleiman Kova amesema kuwa uchaguzi unaendana  na usalama hivyo jeshi limejipanga katika ulinzi katika kipindi hiki.


Kova amesema kuwa Jeshi litaendelea kushirikiana na viongozi wa siasa katika kuleta amani katika kipindi cha uchaguzi.

SHEIN AANDAA MIPANGO NA SERA ZA KUSAIDIA VIJANA ZANZIBAR

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ( Pichani) amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mipango na sera nzuri za kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri wenyewe hasa waliojiunga katika vikundi vya ushirika na SACCOS.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa kuwawezesha Wananchi Kiuchumi na tayari watu kadhaa wameanza kufaidika na Mfuko huo sambamba na kuwapatia mafunzo ya kitaalamu pamoja na kuvipatia vikundi vya ushirika mbinu za kupata masoko na kuwawezesha kuwa wajasiriamali wazuri.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Dk. Shein Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum, Mhe. Haji Omar Kheir, aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa Jumuiya ya Watazania Wasio na Ajira (TUEPO) huko katika ukumbi wa afisi za Jumuiya hiyo Rahaleo, mjini Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa katika kuwasaidia vijana walioshindwa kuendelea na masomo yao, Serikali imeyaimarisha mafunzo ya elimu ya amali katika vituo vya amali vya Mwanakwerekwe na Mkokotoni Unguja na Vitongozi huko Pemba.

Dk. Shein alisema kuwa kituo cha kuwaandaa wajasiriamali katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume imeshaanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kupatiwa mikopo.

Alisema kuwa katika vyuo hivyo vijana hufunzwa ujuzi wa kazi mbali mbali kama vile ufundi umeme, ufundi magari, useremala, uhunzi, kutegengeneza mafriji na amali nyengine ambapo tayari vijana wengi wameweza kunufaika na kujiajiri wenyewe.

Aidha, aliwaeleza vijana hao kuwa mafunzo wanayotoa katika taasisi yao na taasisi nyengine binafsi ni kuongeza fursa za mafunzo ya elimu ya amali kwa vijana ili waweze kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.

Dk. Shein alisema kuwa ukosefu wa ajira nji tatizo linalozikabili nchi zote duniani hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapindyuzi ya Zanzibar zimekuwa zikichukua jitihada mbali mbali katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kushirikiana na jumuiya za Kimataifa, sekta binafsi na jumuiya hiyo ya TUEPO.

“Hivyo kuwepo kwenu hapa ni hatua ya juhudi za pamoja ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote huwa inazishajihisha katika kukabiliana na tatizo la ajira hasa klwa vijana wetu”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua ukubwa wa tatizo la ajira kwa vijana kutokana na uchache wa fursa za ajira serikalini na kuwepo kwa ongezeko la vijana wanaomaliza masomo katika ngazi mbali mbnali kwa kila mwaka na kutegemea ajira ziliopo.

Alisema kuwa inatia moyo kuona hivi sasa, vijana wengi wasomi wameanza kushajihishana kuanzisha vikundi vya ushirika na kujiajiri wenyewe bila ya kuendelea kusubiri ajira Serikalinini.

Dk. Shein aliwanasihi vijana hao kuhakikisha kuwa mafunzo wanayotoa yazingatie ubora na hali ya mahitaji ya soko la ajira sambamba na kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Taasisi mbali mbali za Serikali kama vile Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali yenye dhamana ya kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa kwa wananchi.

 “Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya hii na taasisi zote zinazounga mkono mipango na jitihada mbali mbali za Serikali katika kuleta maendeleo na Ustawi wa wananchi wetu”,alisema Dk. Shein.

Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuzitumia vyema fursa zilizoandaliwa na Serikali pamoja na Taasisi binafsi katika kuwawezesha katika kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya  ya Watanzania Wasio na Ajira (TUEPO) Ussi Said Suleiman alisema kuwa lengo la Jumuiya hiyo ni kuwandaa vijana kielimu kwa kufundisha fani mbali mbali pamoja na kuwatafutia fani mbali mbali ndani na nje ya nchi, ili kuondosha tatizo la ajira.

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa jumuiya inashirikiana na itashirikiana na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali katika kupunguza tatizo la ajira nchini ambapo tayari imeanisha chuo cha Tanzania star teachers college kwa lengo lam kwuasaidia wanachama wa jumuiya hiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio ya Jumuiya hiyo pamoja na changamoto zilizopo, ambapo Waziri Kheir alichangia Tsh. milioni mbili kwa upande wake akiwa kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum.

Jumuiya hiyo imeenzishwa tarehe 23.4.2015 ikiwa na wanachama watano ambapo hadi sasa ina wanachama 210 .

BALOZI DR MAHIGA DAWA SI KUHAMA CCM ASEMA YEYE NI MKOMBOZI WA CCM IRINGA MJINI.

Balozi Dr Mahiga -Iringa mjini.

Na matukiodaimaBlog
ALIYEKUWA balozi wa kudumu  wa umoja  wa mataifa (UN) na mgombea urais katika mchakato  wa ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) balozi Dr Augustono Mahiga anayeomba kuteuliwa kuwa mgombea ubunge jimbo la Iringa mjini kupitia CCM amewashangaa makada  maarufu wa chama  hicho  walioshindwa katika mchakato wa ndani ya chama kwa nafasi ya urais kuhama chama hicho kuwa hao hawakuwa na mapenzi ya kuwatumikia  watanzania na kuwa watazunguka kote ila chama makini ni CCM pekee na kuwataka wana CCM jimbo la Iringa mjini kumpa nafasi yeye ili kuondoa masalia ya Chadema .

Balozi Dr Mahiga  alisema kuwa wana CCM hao  walioanza kuhama chama  kwa kukosa nafasi ya urais hawakuwa na mapenzi mema na CCM bali  walikuwa wawametanguliza  maslahi yao mbele na  kuacha kuangalia maslahi ya Taifa na chama hivyo ni vema watanzania  kuwatazama kwa jicho la tatu na ikiwezekana kuwachunguza japo kwa miaka 5 bila kuwachagua kuwa  viongozi  wao.

Alisema kuwa kama  suala ni uongozi kwa ajili ya  kuwatumikia  wananchi na chama kulikuwa hakuna  sababu ya kuhama chama ama kuanza kutukana chama kwa sasa ila wangeweza  kushuka chini na  kugombea nafasi za chini ukiwemo udiwani ama ubunge kama ambavyo  yeye alivyoshuka na kugombea ubunge ili kuwatumikia watanzania kwa ngazi ya ubunge.

"Kila nafasi ndani ya chama ina maana  kubwa katika kutumikia  watu hivyo kuhama chama si jambo jema na upande wa vyama lazima kuwa makini na wanachama wanaohama vyama kwa sasa ili  kupata nafasi za uongozi iwapo  watakosa nafasi hizo  bila shaka  watachukua hatua ya  kuvuruga nguvu ya vyama  hivyo ama kuhama vyama "

Balozi Dr Mahiga  aliyasema hayo  wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa kuhusiana na mchakato mzima wa kumpata mgombea Urais wa CCM Dr  John Magufuli na mchakato wa kura  za maoni  katika ngazi ya udiwani na ubunge katika  jimbo la Iringa mjini ambako  ni mmoja kati ya  wana CCM 14  wanaoomba kuteuliwa kuwa wagombea wa ubunge .


Alisema akiwa kati ya  wana CCM 41 waliojitokeza  kuchukua fomu ya Urais hana kinyongo na uteuzi wa mgombea  Urais wa CCM Dr Magufuli kwani ni mtu  makini na safi ambae  viatu  vya Rais wa awamu ya nne Dr Jakaya Kikwete ataweza  kuvimudu  vema kutokana na kutokuwa  mtu wa kulipisha  kisasi na hana  makuu na mtu  zaidi ya  kulitumikia Taifa  .

Hivyo alisema iwapo wana CCM  jimbo la Iringa mji watamchagua yeye  kuwa mgombea ubunge  jimbo  hilo wawe imani  ya  kulikomboa jimbo hilo asubuhi  saa 12 kutoka kwa  Chadema  chini ya aliyekuwa mbunge  wa jimbo hilo mchungaji Peter Msigwa kwani alisema  si kweli kama Chadema Iringa mjini wananguvu kubwa kuliko  ya CCM na ukitazama idadi ya wenyeviti wa mitaa ambao CCM inao wenyeviti  104  huwezi linganisha na  wale 64 wa  Chadema kabla ya wenyeviti wake 13 kuvuliwa nafasi zao  na mahakama.

Alisema dawa ya ushindi  wa kishindo kwa CCM Iringa mjini ni moja pekee  kuvunja makundi na kuwa kundi moja la ushindi baada ya zoezi la kura za maoni kumalizika .
Dc Mwamoto  kulia akiwa na mbunge wa Kalenga Godfrey Mgimwa ,mwamoto ni mgombea ubunge Kililo

Mkuu wa wilaya  ya Kaliuwa mkoani Tabora Bw  Venance Mwamoto ambae anawania kuteuliwa kuwa mgombea ubunge  jimbo la Kilolo mkoani Iringa amesema kuwa tishio la  kutaka kuuwawa kwake  majuzi baada ya  kufyatuliwa risasi katika gari lake  wakati akitoka katika kampeni  kata ya  Ilula bado haimtishi  katika safari yake ya  kuwatumikia  wananchi  wa jimbo la Kilolo linaloongozwa na Prof. Peter Msolla .

Kwani alisema moja kati ya ahadi yake  kubwa kwa wananchi wa Kilolo ni  kuona amawatumikia kwa kasi zaidi na kumaliza kero ya maji katika mji  wa Ilula na changamoto nyingine ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa kipindi kilichopita na mbunge  aliyekuwepo .

Mwamoto  alisema kuwa kazi nzuri  aliyoifanya kwa nafasi ya  ukuu  wa wilaya  kwa kipindi  kifupi ambacho  Rais Dr Jakaya kikwete alipomteua kwa  kuwa mkuu  wa wilaya ya  Kibonde na Kaliuwa ni wazi ni  kipimo tosha na heshima kubwa ya wananchi  wa Kilolo kujivunia na  wategemee makubwa zaidi  iwapo  watamchagua kuwa mbunge  wao kwa  sasa .
                                             waziri Lukuvi - Isimani

Mbunge  wa  jimbo la Isimani Bw  Wiliam Lukuvi amewaomba wananchi  wa jimbo  hilo hasa  wanachama wa CCM kuendelea  kujenga imani kwake na kuwa ndani ya CCM kuna Demokrasi  na kila mwanachama ana sifa ya  kugombea nafasi  yoyote ndani ya  chama japo  kipimo  cha kuchaguliwa bado kipo  kwa wananchi  wenyewe ambao  wanaweza kumpima kwa kazi alizofanya badala ya kushawishiwa kwa manenio bila vitendo.

Lukuvi ambae ni waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kama  si wana Isimani kuonyesha ushirikiano  wao kwake na hata  kumchagua katika nafasi hiyo ya  ubunge basi heshima ambayo  ambayo  wana Iringa wameipata  kupitia  wizara yake leo  isingekuwepo .

Alisema suala la migogoro  ya ardhi  amepata  kulishughulikia kwa umaniki mkubwa na kuwa sulaa  hilo pia  lilikuwa ni kero kubwa hata kwa wananchi wake wa jimbo la Isimani ila kwa sasa kwa kiasi  limeanza kupungua na kuwa iwapo wataonyesha imani yao tena  wategemee kuona maendeleo makubwa zaidi katika jimbo hilo na kutaka baadhi ya kazi kubwa ambazo zimefanyika kuwa ni pamoja na barabara ya lami ya Iringa- Dodoma, umeme  vijini , ujenzi wa shule pamoja na ujenzi wa nyumba bora  kwa kupata bati za ruzuku .

"Tumekuwa pamoja  muda  wote katika maendeleo  na matatizo  hivyo lazima  kila  safari ina  wasindikizaji  wake na siku  zote penye maendeleo ndipo panapopendwa na wengi  ila bado kwa tathimini yetu Ismani ya  leo  sio ya jana . nimekomesha ulanguzi wa mazao kama mpunga ,alizeti  kwa kufunga mashine"
                   Godfrey Mgimwa -Kalenga

Mbunge wa jimbo la Kalenga  Godfrey Mgimwa anayeomba kuteuliwa tena kuwa mgombea wa CCM nafasi ya ubunge  amewashukuru wananchi  wa kalenga kwa kuonyesha ushirikiano kwake na kuwa hadi  sasa amepata  kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kwa asilimia 99 na kuwa zipo changamoto mbali mbali ambazo  watampa tena nafasi ya ubunge atakwenda  kuzifanyia kazi .

Mgimwa ambae  amepata  kuongoza jimbo hilo kwa mwaka mmoja pekee akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dr Wiliam Mgimwa aliyefariki duni mwaka jana mwanzioni ,alisema zilikuwepo ahadi mbali mbali ambazo ziliachwa na mbunge aliyepita na tayari zote amezikamilisha kwa kipindi cha mwaka mmoja na kubwa anajivunia kuanzisha vikundi vya Vicoba  zaidi ya 60 ,ujenzi wa barabara , maji  vijiji ,umeme na uchangiaji wa ujenzi wa zahanati ,shule  na maabara na kuwa zaidi ya Tsh milioni 100 amepata  kutumia kwa kuchangia miradi ya maendeleo jimboni.

ASKARI WA TANAPA ASHINDA TUZO YA ULINZI WA FARU BARANI AFRIKA

Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa)Daraja la Pili,Malale Patrick Mwita akiwa ameshika Tuzo na Cheti alivyokabidhiwa na Mwana wa Mfalme Albert wa Pili wa Monaco nchini Afrika Kusini wiki iliyopita katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya Tanapa jijini Arusha.
Meneja Mawasiliano wa Tanapa,Pascal Shelutete akitangaza ushindi wa Tuzo hiyo akiwa na maafisa wa Shirika hilo  ambao wana jukumu la kuhifadhi maliasili kwaajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Meneja Mawasiliano wa Tanapa,Pascal Shelutete akitangaza ushindi wa Tuzo hiyo ambayo imeipa heshima Tanzania katika mapambano yake dhidi Ujangili nchini.

Mwandishi wetu,Arusha
Askari Daraja la Pili ,Malale Patrick Mwita kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti ameshinda Tuzo ya kila mwaka ya Askari Bora katikaulinzi wa Faru kwa mwaka 2015 barani Afrika inayojulikana "2015 Rhino Conservation Awards"

Meneja Mawasiliano wa Tanapa,Pascal Shelutete ametangaza ushindi  huo leo katika ofisi za Makao Makuu ya Tanapa jijini Arusha.

Amesema Tuzo hiyo amekabidhiwa na Mwana wa Mfalme Albert wa Pili wa Monaco ambaye ni mlezi wa Tuzo hizo ambazo washindi walikabidhiwa Julai 27 mwaka huu nchini afrika Kusini.

Askari huyo ameibuka mshindi miongoni mwa washindani wengine kutoka nchi zote za Afrika zenye miradi ya kuendeleza Faru katika  ambapo Tuzo hizo hutolewa kila mwaka baada ya taasisi hiyo kutambua matendo ya kijasiri yaliyofanywa na askari huyo.

Baadhi ya matukio ya kijasiri yaliyofanywa na askari huyo ni askari pekee mwenye uwezo wa kuwatambua Faru zaidi ya asilimia 90  ndani ya Hifadhi ya Serengeti kwa kutumia alama za asili wakati mwaka 2007 alizuia tukio la kuuwawa kwa Faru na mwaka 2008 alishiriki kukamata silaha  5 za kivita. 

Amesema mradi wa Faru wa Moru,serengeti ndio mradi mkubwa kabisa wa faru wenye mafanikio barani Afrika unaoongoza kwa kasi ya kuzaliana ambayo ni zaidi ya asilimia 5 kwa mwaka.

Tuzo hizo huandaliwa pamoja Wizara ya Mazingira ya Afrika Kusini ambayo inahusika na Utalii.

Malale amesema Tuzo hiyo imempa hamasa ya kutambua mchango wa askari katika kukabiliana na majangiri hatari wanaotumia silaha za kivita kwaajili ya kuwinda Faru na Tembo .

"Tuzo hii ni heshima kubwa kwa Tanapa na nchi yetu kwa ujumla katika kuhakikisha tunawalinda wanyama hawa ambao wako katika hatari ya kutoweka kila mmoja wetu ni mdau muhimu kuhakikisha Faru anaishi."amesema Mwita.

FILIKUNJOMBE; MAFISADI WAMETUMA WATU WANING'OE UBUNGE NAOMBA WANANCHI WANYIMENI KURA

mbunge  wa Ludewa  Deo Filikunjombe kulia akiwa na mlemavu wa ngozi (ALBINO) mara  baada ya kumaliza mkutano wake wa kampeni za ubunge 

Na Matukiodaima Blog Ludewa
WAKATI wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM)  kesho   wanashiriki  zoezi la kupiga kura  za maoni kuwapata  madiwani na  wagombea  watakao gombea kwa CCM ,mbunge  wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe amewashukuru wanachama wa CCM  katika jimbo hilo kwa kuonyeha  imani kubwa kwake  ukilinganisha na wagombea  wenzake  wawili na kuwa hadi  sasa anauhakika mkubwa wa kushinda tena ila ushindi utakaompa heshima ni ule wa kupata kura zote na wenzake kuambulia patupu

Filikunjombe  aliyasema hayo   wakati wa mkutano  wa kujinadi kwa  wagombea wa nafasi ya  ubunge katioka kata ya Ludewa mjini ,kuwa hadi  sasa kutokana na mapokeo  ya wananchi na  wana CCM kote walikopata kupita kwenye kata 26 za  jimbo hilo la Ludewa wamekuwa wakitamka  bayana kuwa kura  zote kwake  hivyo  kuwaomba wana CCM kwa umoja  wao kumpa moyo zaidi wa kuwatumikia tena kwa kuhakikisha  wanampatia kura  zote za ndio.

Alisema kwa kauli zao wagombea wenzake wawili  waliojitokeza wanaeleza bila kuficha kuwa wametumwa na watu  ambao  aliwaondoa bungeni kutokana na vitendo vyao vya ufisadi  ili  waje Ludewa  kugombea ubunge kwa ajili ya kulipa kisasi kwa kumtoa jambo ambalo hadi sasa  limegonga mwamba kutokana na wananchi na wana CCM Ludewa kuliona hilo.

"Niliifanya kazi  ile ya  kupambana na mafisadi bungeni kwa faida ya  wananchi wa Ludewa na watanzania kwa ujumla ila nashangazwa  kuona  leo wana Ludewa wachache wanakubali  kutumika na mafisadi hao kutumwa kuja kunitoa ubunge kweli ni aibu  kubwa kwa kazi kubwa ambayo mimi nimeifanya katika  jimbo la Ludewa  sikutegemea kupata mpinzani tena ndani ya chama changu.....ila naomba sana  wana Ludewa  tuungane katika vita  hii ya maendeleo na kupinga ufisadi kwa kuwanyima kura hawa "

Alisema kuwa wilaya ya  Luudewa itajengwa na wana Ludewa kwa kushirikiana na yeye kama mbunge wao na sio wale wanaotumika  kuwadanganya wananchi wa Ludewa hata kupinga kazi kubwa iliyofanyika kwa kipindi kifupi cha miaka mitano .

Filikunjombe  alisema kuwa hawezi kusema kuwa amemaliza changamoto  zote za wilaya hiyo ya Ludewa kwani kama atasema hivyo atakuwa anawadanganya  wananchi wake na kuwa pamoja na kuwa amefanya mengi ila hajamaliza changamoto  zote za jimbo la Ludewa hivyo iwapo  watampa tena nafasi hiyo ua ubunge atahakikisha anaendelea kupunguza changamoto zilizobaki.

" nimefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo jimbo la Ludewa ila nitakuwa nadanganya kama nitasema nimemaliza changamoto  zote pia hata wabunge  wenzangu walifanya kulingana na wakati  ule  na kila mmoja a namchango  wake katika  maendeleo ya Ludewa .....ninachowaomba wananchi mtupime  wagombea kwa kazi  tulizofanya msitupime kwa maneneo kwangu mimi ni kazi zaidi maneno kidogo"

Hata  hivyo alisema iwapo wananchi  wa kata ya  Ludewa watamchagua kuwa mbunge kwa kura za kishindo atahakikisha kero ya maji anaanza kuitatua kabla ya  serikali kuanza kufanya hivyo kwani kati ya changamoto kubwa kwa mji wa Ludewa ni pamoja na maji .

Pia  aliwataka  wananchi kupuuza  uongo unaosambazwa na wagombea hao kuwa  vikao vya juu vya chama vimepanga  kukata  jina lake  baada ya  kushindwa na kudai kuwa huo ni upotoshaji na kuwa CCm ni chama makini na hakuna mtu wa kukatwa iwapo ametekeleza sera  vema za chama.

Huku mgombea injinia Zephania Chaula akiwaomba  wananchi hao kumchagua kuwa mbunge kwani tayari ameahidiwa na  na mwenyekiti wa DP mchungaji Christopher Mtikila na aliyekuwa mbunge wa  jimbo hilo kabla ya  kuangushwa na mbunge filikunjombe mwaka 2005 Prof Raphael Mwalyosi kuwa watamsaidia  kufanya kazi pamoja .

Chaula ambae  alipingwa vikali katika mkutano huo kiasi cha kuzomewa baada ya kudai moja kati ya kazi aliyoifanya ni kuanzisha  mfereji wa umwagiliaji kata ya  Ruhuhu baada ya mkazi wa kata  hiyo aliyekuwepo mkutanoni hapo kunyosha mkono na kumpinga kuwa hakuna mradi huo ni uongo na kuwa wao  wanamtegemea mbunge wao Filikunjombe ambae amefanya mengi kwenye kata  hiyo.

Wakagti Injinia Chaula ambae  siku za hivi karibuni aliambulia kura  11 katika nafasi ya ujumbe wa NEC akipingwa  vikali mkutanoni hapo mgombea Kepten (mstaafu) Jacob Mpangala akijikuta katika wakati mgumu kufuatia mbunge Filikunjombe kuwasilisha vielelezo sahihi mbele ya viongozi wa chama na kugawa kwa wananchi hao viinavyoonyesha mgombea  huyo anavyodanganya  wananchi  kuwa alistaafu kazi wakati kuna barua ya  kufukuzwa kwake kazi kutoka TAMISEMI.

Filikunjombe alifikia hatua  hiyo ya  kukabidhi  ushahidi huo kwa chama baada ya kauli ya  vitisho ya mgombea  huyo Mpangala kumtaka aonyeshe hadharani ushahidi unaoonyesha kufukuzwa kakwe kazi kabla ya kuchukua hatua .

MKURUGENZI WA MTENDAJI WILAYA YA HANANG' AKANUSHA TUHUMA ZA HALMASHAURI YAKE KUTAFUNA FEDHA ZAIDI YA TSH MILINIONI 500


Na woinde shizza.
MKURUGENZI mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara,

Filex Mabula amesema taarifa zilizotolewa kuwa halmashauri hiyo imetumia

vibaya zaidi ya sh508.6 milioni fedha za shule na za kusambaza maji
vijijini, zilizotolewa na benki ya dunia, siyo za kweli.



Akizungumza na waandisi wa habari jana, Mabula alisema halmashauri hiyo

ilitoa sh225.5 milioni kwenye shule za bweni kwa ajili ya chakula kwa mwaka 2013 hadi 2014 sawa na asilimi 281.9 ya fedha zilizoidhinishwa na hazina.



Fedha zetu zinatumika kwa kufuata kanuni na taratibu ndiyo sababu mkuu wamkoa wetu Joel Bendera alitupongeza Hanang’ kwa kupata hati safi kwa maraya nne mfululizo kupitia ukaguzi wa ripoti ya CAG,” alisema Mabula.


Alisema sh283.1 milioni zilipelekwa kwenye shule za Katesh, Balang’dalalu,

Bassodesh na Gendabi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya shule na kamati ya
fedha iliidhinisha kwa kikao cha Juni 26 mwaka huu na baraza la madiwani
Julai 8. 


Alisema vijiji saba vya Getasam, Ng’alda, Gidagharbu, Simbay, Ishponga,

Garawja na Galangal, vimepatiwa miradi ya maji kupitia ufadhili wa benki ya dunia na vijiji vya Hirbadaw, Wandela na Dajameda vitanufaika hivi
karibuni. 



Wanasiasa msiwakatishe tamaa watendaji bila sababu ya msingi kwa kutumia kipindi hiki cha uchaguzi kuwapotosha wananchi kwani kiongozi bora anapatikana kwa utendaji wa kazi siyo kudanganya jamii,” alisema Mabula.


Nao, baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo walipongeza jitihada zinazofanywa na uongozi wa halmashauri hiyo kupitia mkurugenzi huyo Mabula kwani miradi mingi ya maendeleo imefanikiwa na jamii inanufaika nayo.

Mkazi wa Katesh, Julius Gidang’ai alisema mara nyingi wanasiasa wamekuwa wakikwamisha miradi mingi ya maendeleo kutokana na kuzusha vitu vya uongo endapo baadhi ya miradi ya maendeleo itakapokuwa haijazifikia kata zao.



Hivi sasa sisi wananchi wa kata ya Endasak tumeshindwa kuendelea na mradi wetu wa umwagiliaji kule Endagaw baada ya Mabula kusimamia zoezi vizuri lakini wanasiasa wakakwamisha,” alisema Zainab Juma mkazi wa kijiji cha Endagaw.

SHEREHE ZA NANE NANE KANDA YA KATI KUFANYIKA VIWANJA VYA NZUGUNI MKOANI DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa akiwasilisha taarifa ya
maandalizi ya sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati zitakazo fanyika
sambamba na Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Kitaifa kuanzia Agosti
Mosi Mkoani Dodoma.

Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati zitafanyika sanjari na Maonesho na mashindano maalum ya mifugo ya 5 Kitaifa  katika  uwanja wa Nzuguni Dodoma kuanzia tarehe 01/08 hadi 08/08/2015.

Sherehe za Nane Nane mwaka huu 2015 zinakwenda kwa Kaulimbiu inayosema “Matokeo Makubwa sasa  (BRN)– Tuchague viongozi bora kwa maendeleo ya Kilimo na Ufugaji” Kaulimbiu hii imekuja wakati muafaka ambapo Taifa letu la Tanzania linaelekea katika Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba na tayari baadhi ya vyama vya siasa vimeshaanza mchakato wa kuendesha kura za maoni ili kupata wagombea wa nafasi mbalimbali.

Kaulimbiu hii inatoa msisitizo kwa wananchi na watanzania wote kuchagua viongozi bora ambao watasaidia kuleta matokeo makubwa sasa katika nyanja za Kilimo na Ufugaji kwa maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla.

Kama ilivyo ada,  Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati sanjari na Maonesho na mashindano maalum ya mifugo Kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Nzuguni hapa Dodoma, yameendelea  kuwa kitovu na chemchem ya elimu juu ya:  
  • Zana bora za Kilimo na Mifugo
  • Pembejeo za Kilimo na Mifugo
  • huduma za Mawasiliano ya Kibiashara
  • Usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo
  • taasisi mbalimbali za Fedha na Mabenki
  • Mafunzo na Utafiti na
  • taasisi za uzalishaji za Serikali.

Hadi kufikia sasa maandalizi muhimu kwa ajili ya kufanikisha Sherehe hizi za Nane Nane yapo katika hatua nzuri.

Maendeleo ya Vipando na Mabanda ya Mifugo kwa ujumla yapo katika hatua nzuri ingawaje hatua iliyofikiwa inatofautiana kati ya taasisi na taasisi.

Miundombinu ya Barabara Inapitika kirahisi, TASO kwa kushirikiana na Kamati ya Maandalizi ya Nane Nane Kanda ya Kati  inaendelea kufanya usafi wa barabara na kuhakikisha zinakuwa katika hali nzuri wakati wote wa Maonesho.

Huduma ya Maji inategemea mtandao wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dodoma (DUWASA) ambao ndiyo unaotumiwa na wadau wengi na visima virefu (9) ambavyo vimechimbwa  na wadau kwa matumizi yao. TASO Kanda ya Kati inaendelea kushughulikia changamoto ya kiufundi na kukatika kwa umeme kwa lengo la kuhakikisha maji hayakosekani kwenye viwanja vya Nane Nane Nzuguni.

Arena ya Mifugo imefanyiwa usafi na marekebisho madogo ili kuboresha mashindano maalum ya mifugo ya 5 Kitaifa. Kwa upande wa Mabanda ya Maonesho, Napenda kutoa wito kwa Wizara, Taasisi za Serikali, Taasisi zisizo za serikali , asasi na wadau mbalimbali kuendelea kukamilisha ujenzi wa mabanda yao ya maonesho kwenye viwanja vya Nzuguni ili kuleta ufanisi wa shughuli za Nane Nane.

Washindi wa Maonesho ya uwanjani: (Wakulima na Wafugaji bora) Kutakuwa na Majaji wasiopungua wanne (4) kutoka hapahapa Kanda ya Kati na  baadae washindi wa Maonesho watapewa zawadi kulingana na hali ya fedha, naomba nisitaje hapa  lakini niweke wazi kuwa Jukumu la kutoa zawadi ni la Kamati ya Maandalizi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Natumia fursa hii kuwakaribisha wakulima na wafugaji kutoka mikoa ya kanda ya kati na maeneo mengine ya Nchi, Wadau mbalimbali kuja kushiriki maonesho haya ya Nane Nane na pia nawakaribisha wananchi hususani wakulima, wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali kuja kwa wingi kutembelea Maonesho ya Nane Nane na Maonesho na Mashindano maalumu ya mifugo kwenye viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma kuanzia tarehe 1-8 Agosti, 2015 ili waweze kujifunza.

Kwa muhtasari matukio makuu kwa mujibu wa ratiba, katika siku ya ufunguzi na Kufunga Msisitizo utakua Kaulimbiu ya Maonesho, Siku ya Pili ya Maonesho Msisitizo utakua kuona Kiwango cha teknolojia ya Uzalishaji wa bidhaa za kilimo , mifugo, maliasili na viwanda katika kukuza uchumi.

Siku ya tatu ya Maonesho Msisitizo utakuwa Serikali za Mitaa kusimamia maendeleo vijijini; Siku ya nne msisitizo utakua juu ya sera ya mikopo kwa wakulima na wafugaji wadogo. Siku ya tano itahusisha Ufunguzi wa Maonesho na mashindano Maalumu ya tano (5) ya mifugo. Siku ya sita ya Maonesho msisitizo utakuwa kwenye umuhimu wa habari kwa maendeleo ya kilimo na mifugo. Siku ya saba msisitizo utakuwa kwenye Hifadhi ya Mazingira kwa kilimo na ufugaji endelevu.

Nawakaribisha sana wananchi na wadau mbalimbali wa kilimo na mifugo hapa Dodoma na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye Maonesho ya Mwaka huu, niweke mkazo kuwa ulinzi na usalama umewekwa vizuri ili kuhakikisha Maonesho hayo yanafanyika salama kwa utulivu na amani.

Katika hatua nyingine, kila Mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine kuadhimisha ”Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani.” Maadhimisho haya yaliyoanza mwaka 1992, hufanyika kuanzia tarehe 01 – 07/08 ya kila mwaka.

Kwa mwaka huu 2015, Mkoa wa Dodoma Makao Makuu ya Nchi, umepewa heshima ya kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama kitaifa. Maadhimisho haya yatakwenda sanjari na Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati na Maonesho na mashindano maalum ya mifugo ya 5 Kitaifa. Maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia  Julai 1 - 7, 2015, ufunguzi utafanyika kwenye wilaya ya Chamwino kwenye Kijiji cha Nkwenda, wakati sherehe za Kilele cha Maadhimisho hayo Kitaifa zitafanyika hapa Manispaa ya Dodoma kwenye viwanja vya Maonesho ya Nane Nane Nzuguni.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama  mwaka huu ni ”UNYONYESHAJI NA KAZI: TUHAKIKISHE INAWEZEKANA” (Breastfeeding and Work Lets Make it Work). Kaulimbiu hii inalenga kuwasaidia wanawake WOTE wanaofanya kazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi waweze kutunza watoto wao ipasavyo pamoja na kufanya kazi mathalani kuajiriwa, kujiajiri, kazi za muda mfupi au mikataba na kazi zisizo za kulipwa kwa mfano kazi za mazingira ya nyumbani, shamba, mifugo na kutunza familia.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, pamoja na masuala mengine muhimu, kutakuwa na utoaji wa elimu ya lishe kwa njia za vyombo vya habari, elimu ya lishe kwenye vituo vya kutolea huduma na eneo la Nane Nane, elimu ya lishe na unyonyeshaji kwa makundi ya wanafunzi, viongozi na Uhamasishaji kwa njia ya gari la maonesho na semina.

Hivyo natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa ya jirani kuhudhuria ufunguzi na kilele cha maadhimisho haya ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Kitaifa, halikadhalika, kutumia fursa hii adhimu kupata elimu juu ya masuala ya Unyonyeshaji na lishe ili kusaidia kumaliza tatizo la Utapiamlo baina ya wanawake walio katika umri wa kuzaa (15 – 49 yrs) halikadhalika kuondoa tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri wa miezi 6 – 59.
                                             
Imetolewa na:
OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA
Julai 30, 2015.